WIZARA YA AFYA YAANDAA MPANGO WA KUSOMESHA MADAKTARI BINGWA NA WABOBEZI.
Na Wellu Mtaki, Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imetoa ufadhili wa shilingi bilioni nane kwa kuwasomesha madaktari bingwa na wabobezi ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari.
Waziri Ummy amesema mpango huo unaojulikana kama Samia Scholaship utasomesha madaktari ngazi za ubingwa 139 watasoma nje ya nchi na wengine 318 watasomea hapa nchini.
Mwalimu amesema kuwa mpango huo utakuwa ni kwa seti akitolea mfano daktari bingwa wa magonjwa ya figo atakwenda kusoma pamoja na muuguzi na mtaalamu wa dawa ya usingizi ambapo jumla watakuwa watatu katika ugonjwa mmoja.
Amefafanua kuwa katika mpango huo tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameikabidhi Wizara ya afya kiasi cha shilingi bilioni nane ambazo zitatumika kama ada na posho nyingine watakapokuwa mafunzoni.
Ameongeza kuwa Serikali imeamua kufanya hivyo baada ya kuona nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa huduma za kibingwa na ubobezi.