Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu waliokuwa
wamepakizana kwenye pikipiki moja wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu wakiwa
wamevalia hijabu wameuwawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kukaidi amri
ya kutakiwa kusimama.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake mjini Kibaha Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga
alisema kuwa pikipiki nyingine mbili zilifanikiwa kukimbia.
Lyanga akielezea juu ya tukio
hilo alisema kuwa lilitokea Aprili 2 mwaka huu majira ya saa 12:00 mchana eneo
la kizuizi cha Mwembe Muhoro wilaya ya Rufiji mkoani Pwani barabara kuu ya Dar
es Salaam Lindi.
“Siku ya tukio askari walipata
taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini
zikiwa zimebeba watu watatu kila moja huku miongoni mwa pikipiki hizo kati yake
mbili wamebebwa watu waliovaa hijabu,” alisema Lyanga.
Alisema kuwa askari wa
barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha Mparange na kuwasimamisha ili
wawahoji lakini walikataa na kupita ambapo waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi
cha Ikwiriri lakini walikaidi kusimama.
“Baada ya hapo walifika kizuizi
cha Ikwiriri lakini bado walikaidi kusimama na kuendelea kukimbia ndipo
walipofika kituo cha Muhoro hata hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria
wakiwa kwenye gari waliwafuatilia wakijaribu kuwafuatilia na wakavuka daraja la
Mkapa na waliwapa onyo kwa kupiga risasi hewani,” alisema Lyanga.
Aidha alisema kuwa baada ya hapo
watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza kukimbilia msituni na ndipo askari
walipowapiga risasi za miguu na kiunoni na kufanikiwa kuwakamata.
“Majeruhi hao walijulikana ni
wanaume hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika na walikuwa kwenye pikipiki
yenye namba za usajili MC 272 BLW aina ya Boxer yenye rangi nyeusi ambapo watu
hao wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha
Hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alisema Lyanga.
Lyanga alisema kuwa walipofikishwa
hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao wamefariki dunia ambapo hata
hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku pikipiki nyingine mbili zilitoroka
na kuelekea mkoa wa Lindi na taarifa zimetolewa polisi ili wawakamate.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu
pale wanaposimamishwa na askari polisi badala ya kujaribu kutoroka na kwa sasa
jeshi hilo limeimarisha doria katika kukabiliana na uhalifu.
Mwisho.