Na John
Gagarini, Mkuranga
WANANCHI
wametakiwa kuwa na utamaduni wa kulipa kodi mbalimbali za serikali ili ziweze
kutumika kwa ajili ya maendeleo kama wanavyofanya wananchi wa Libya.
Hayo yalisemwa wilayani
Mkuranga na mkurugenzi wa Taasisi ya World Islamic Call Society iliyopo chini
ya ubalozi wa Libya hapa nchini Ammara Zaiyani wakati akikabidhi mradi wa kisima
cha maji kwenye Kijiji cha Binga–Kisiju.
Zaiyani alisema
kuwa fedha ambazo zimesaidia ujenzi wa kisima hicho cha maji ya kunywa chenye
thamani ya shilingi milioni 18 zimetokana na kodi za wananchi wa Libya kwa ajili
ya kusaidia watu wenye changamoto mbalimbali za kimaendeleo.
“Wananchi wa
Libya wanajitolea kuwasaidia wenzao hivyo na nyie mnapaswa kuwa na utamaduni wa
kuwasaidia wengine kupitia kwenye malipo mbalimbali ya serikali yenu ambayo ina
sema hapa Kazi Tu,” alisema Zaiyani.
Naye mwakilishi
wa Ubalozi wa Libya hapa nchini Mohamed Atoumi alisema kuwa serikali ya Libya
kupitia taasisi hiyo imekuwa ikipokea maombi mbalimbali na imekuwa ikisaidia
kadiri ya uwezo unapokuwepo.
Atoumi alisema
kuwa wamekuwa wakisaidia kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja kwenye huduma
za afya, maji na shughuli nyingine za maendeleo lengo likiwa ni kudumisha
ushirikiano uliopo na Tanzania.
Kwa upande wake
kadhi mkuu wa mkoa wa Pwani Sheikh Hamis Mtupa alisema kuwa wanashukuru kwa
msaada huo kwani umesaidia kuwaondolea adha wananchi wa Kijiji hicho ambao
walikuwa wakishinda wakitafuta maji ambayo siyo safi wala salama.
Mtupa alisema
kuwa wananchi wanapaswa kulinda miundombinu ya kisima hicho ili isiharibike
kwani maji hayo ni kwa wananchi wote bila ya kujali dini ya mtu na ni huduma
muhimu kwa binadamu.
Naye mkazi wa
kijiji hicho Mwanahawa Maulid alisema kuwa wamekuwa wakihangaika kutafuta maji
ambayo yanapatikana mbali na wamekuwa wakitumia muda mwingi kusubiria maji.
Maulid alisema
kuwa maji waliyokuwa wakiyatumia ni ya kuchimba chini ambayo si salama kiafya
na yamekuwa wakiwasababishia magonjwa mbalimbali kama vile kuhara na UTI.
Mwisho.