Friday, June 20, 2014

SARE ZA JESHI NA BASTOLA VYADAKWA

WATATU WADAKWA NA SILAHA NA SARE ZA JESHI

Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limefanikiwa kuwakamata watu watatu akiwemo mtu Daniel Mtalisi mkazi wa Kisemvule wilaya ya Mkuranga ambaye alipitia mafunzo ya kijeshi kwa tuhuma za kufanya tukio la uhalifu wa kupora silaha na vitu mbalimbali.
Mtuhumiwa huyo ambayealiwahi kupata mafunzo ya kijeshi kwenye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi namba 833 Oljoro Arusha na namba yake ni MT. 95150.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa waandishi wa habari mjini Kibaha, kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP) Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 17 mwaka huu majira ya saa 2 usiku huko Kijiji cha Kisemvule kata ya Vikindu kata ya Mkuranga wilaya ya Mkuranga.
Kamanda Matei alisema kuwa watuhumiwa hao wengine wakiwa ni Khalfan Abas (25) mkazi wa Mwanambaya na Mashaka Masanja (24) mkazi wa Mwongozo Kigamboni Jijini Dar es Salaam walikamatwa baada ya polisi kufanya msako mkali na kumkuta mtuhumiwa huyo akiwa na silaha hiyo ambayo walimpora Musa Kambangwa ambaye ni mfanyabiashara wa Mwanambaya.
“Watu hao walimvamia mlalamikaji ambaye alikuwa akirejea nyumbani kutoa kwenye biashara zake walimteka kisha kumpiga na walimwamuru awapeleke nyumbani kwake na kuichukua silaha hiyo bastola yenye namba A 569542 aina ya Browning, Carriber 7.65 mm, magazine 2 na risasi 23, chaja 1 ambavyo alikuwa amehifadhi nyumbani kwake,” alisema Kamanda Matei.
Aidha Kamanda Matei alisema kuwa kabla ya kukamatwa watuhumiwa hao walifanya tukio hilo Juni 11 mwaka huu huko Kijiji cha Mwanambaya ambapo walimvamia mlalamikaji akiwa na mke wake.
“Walimjeruhi kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi na kumsababishia maumivu makali kisha kumtaka awape funguo ya nyumba yake ili waingie ndani lakini alikataa wakaendelea kumpiga hadi alipopoteza fahamu na kuichukua funguo na kuingia ndani na kuchuakua silaha hiyo na simu 2 aina ya Nokia, Inveta , deki 1 ya Dvd  na viatu pea moja kisha kutoweka na ndipo walipokuja kukamatwa Juni 17,” alisema Kamanda Matei.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo ndipo walipofanya msako na kufanikiwa kuvikuta vitu hivyo ambapo mtuhumiwa wa kwanza alikutwa na sare za Jeshi.
Alibainisha kuwa mlalamikaji anaendelea vizuri na kuwataka watu kutoa taarifa za uhalifu ili kuzuia matukio hayo ambayo yameanza kuibuka kwa wingi na watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi wa tukio hilo utakapokamilika.
Mwisho      

Monday, June 16, 2014

WANAJESHI WAWILI WAFA AJALINI



Na John Gagarini, Kibaha
WATU wawili wamefariki dunia huku mmoja akijeruhiwa baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani Pwani, kamishna Msaidizi mwandamizi wa polisi (SACP) Ulrich Matei amesema kuwa ajali hiyo ilihusisha lori na gari dogo.
Kamanda Matei alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Juni 16 mwaka huu majira saa 1:15 usiku eneo la Chamakweza kata ya Pera tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
Alisema ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 164 AUS na tela namba T 498 AZ likiendeshwa na Hassan Shaban mkazi wa Dar es Salaam ambaye aligongana na gari aina ya Isuzu Carry lenye namba za usajili Z 190 DR likitokea mkoani Morogoro.
“Waliokufa ni  dereva wa gari dogo Meja Edward Mosi ambaye ni ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha Kinonko na mkaguzi Msaidizi wa Polisi wa wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Johnson Zakaria,” alisema Matei.
Aidha alisema katika ajali hiyo mtu mmoja alijeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kwa ajili ya matibabu huku miili hiyo nayo ikiwa hospitalini hapo kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.
“Kutokana na ajali hiyo jeshi la polisi linamtafuta dereva wa lori ambaye alikimbia mara baada ya tukio hilo, ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Matei.
Mwisho.