Friday, May 20, 2022
KEDA YATOA MSAADA WA MARUMARU ZA MAMILIONI KWENYE SHULE ZA SEKONDARI
KIWANDA cha kutengeneza Marumaru cha Keda (T) Ceramics Co. Ltd kilichopo Pingo Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kimetoa Marumaru zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 kwa shule za Pera na Msata.
Akizungumza mara baada ya kuzikabidhi shule hizo Ofisa Tawala wa kiwanda hicho George Lulandala alisema kuwa maramaru hizo ni kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya usomaji kwa wanafunzi.
Lulandala alisema kuwa wametoa vifaa hivyo ikiwa ni sehemu ya kurudisha mchango wao kwa jamii ambapo wamekuwa wakishiriki shughuli za wananchi ili kuwaletea maendeleo.
"Tumeamua kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwani ameonyesha kuwajali wananchi wakiwemo wanafunzi ambapo amefanya mambo mengi kwenye sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa na miundombinu,"alisema Lulandala.
Alisema kuwa wameamua kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha mazingira ya elimu ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri ambayo yatawafanya wapate uelewa vizuri.
"Sekondari ya Msata imepatiwa maboksi 203 huku Pera Sekondari wakipata maboksi 100 na bado tutaendelea kutoa misaada mbalimbali ili kuhakikisha kuboresha sekta mbalimbali,"alisema Lulandala.
Aidha alisema kuwa kwa kipindi cha nyuma walisaidia kituo cha afya cha Pera na huduma mbalimbali kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali kwenye wilaya na mkoa.
"Tunafanya jitihada mbalimbali kusaidia masuala ya jamii hivyo hata wadau wengine nao wanapaswa kuisaidia serikali ili iweze kuwahudumia wananchi wake,"alisema Lulandala.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Iddi Ng'oka alisema kuwa wanashukuru kiwanda hicho kwa msaada walioutoa kwani bila ya kuweka Marumaru sakafu imekuwa ikiharibika mara kwa mara.
Ng'oka alisema kuwa wanaomba wapewe tena maramaru kwani kuna baadhi ya madarasa hayana Marumaru pamoja na ofisi hivyo wakipatiwa nyingine itasaidia sana.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)