Wednesday, September 6, 2017

WATATU WAFA WAKITOKA BUNGENI DODOMA KUSHUHUDIA KUAPISHWA WABUNGE VITI MAALUMU CUF

Na John Gagarini, Kibaha
WATU watatu wamefariki dunia huku wengine watatu wakijeruhiwa walipokuwa wakitokea Bungeni mkoani Dodoma kushuhudia kuapishwa kwa wabunge saba wa Viti Maalumu wa Chama Cha Wananchi (CUF) baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na lori la mizigo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa watu hao walifia papo hapo.
Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 6 majira ya saa 8:30 usiku eneo la Kijiji cha Ubena Zomozi barabara ya Dar es Salaam-Morogoro wilaya ya Kipolisi Chalinze-Bagamoyo.
“Gari lililokuwa limetoka Dodoma kwenda Muheza mkoani Tanga ni aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 968 CSK likiendeshwa na dereva Uled Sarumaa (32) mkazi wa Muheza liligongana na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 929 CBK lenye tela namba T 472 CAX lililokuwa likiendeshwa na Yasin Kanoni (35) mkazi wa Jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo hivyo,”alisema Shana.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni dereva wa Noah Sarumaa, Mary Komba (40) mkulima mkazi wa Muheza na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Isaack mfanyabiashara anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (37).
“Majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Juma Nindi (47) mfanyabiashara wa Muheza, Chausiku Hassan (47) mkulima wa Muheza na Ester Mafie (67) mkulima mkazi wa Muheza,” alisema Shana.
Aidha alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kusubiri uchunguzi wa daktari na kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi huku majeruhi wakiwa wamelazwa kituo cha afya cha Chalinze
Alibainisha kuwa na chanzo cha ajali kinachunguzwa na alipoulizwa juu ya waliokufa kama ni viongozi wa CUF amesema kuwa bado hajapata taarifa kuhusiana na hilo pia dereva wa lori Yasin Kanoni alikimbia mara baada ya tukio hilo na kwa sasa anatafutwa.
Mwisho. 

BABA WA KAMBO AMJERUHI MTOTO KWA KUIBA MAYAI MAWILI





Mtuhumiwa Abdala Machupa akiwa kituo cha Polisi Kongowe
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi Mkoani Pwani linamshikilia Abdala Machupa (49) fundi ujenzi mkazi wa Kongowe kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kumkata na kisu kichwani mwanae wa kufikia (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka (5) mwanafunzi wa shule ya awali ya Kongowe Kati kwa madai ya kuiba mayai mawili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kamanda wa Polisi mkoani humo Jonathan Shana alisema kuwa mtuhumiwa huyo alipata taarifa hizo mitaani za mwanae kuiba mayai hayo.
Kamanda Shana alisema kuwa  mtoto huyo alitutuhumiwa kuiba mayai kwa Bibi Baby Septemba 4 majira ya saa 2 usiku na kumfiki mama yake mzazi aliyefahamika kwa jina moja la Hadija ambaye alimkanya mwanae kwa kumchapa viboko.
“Mnamo Septemba 5 mtuhumiwa huyo alipata taarifa mtaani kuwa mtoto wake kaiba mayai alirudi nyumbani na kuanza kumchapa kwa fimbo na kama haitoshi alichukua panga lakini mwanae mwingine Hamis Abdala miaka (8) akamzuia ndipo alipochukua kisu na kumkata kichwani mara mbili,” alisema Shana.
Alisema kuwa wananchi baada ya kupata taarifa walifika na kuingilia kati ili kumwokoa mtoto huyo na wao ndipo walipomshambulia na kumjeruhi kichwani na kisogoni kisha walimfikisha polisi.
“Mtuhumiwa alipatiwa matibabu na kwa sasa bado yuko mahabusu na amekemea tabia ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto ambapo upelelezi umekamilika na mtuhumiwa alitarajiwa kufikishwa mahakamani jana,” alisema Shana.
Awali akizungumzia juu ya tukio hilo mwenyekiti wa mtaa wa Bamba Amri Mavalla alisema kuwa wakati mtuhumiwa huyo akimwadhibu mama mzazi wa mtoto huyo ambaye ni mjamzito alipoteza fahamu kwa hofu kwa mwanae.
Mavalla alisema kuwa aliletewa taarifa majira ya saa 6 ofisini kwake na ndipo alipokwenda kupata taarifa juu ya tukio hilo ambapo mama mzazi wa mtoto huyo alishindwa kuchukua yoyote wakati baba yake akimwadhibu kutokana na hali yake.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo wasamaria wema walimpa huduma ya kwanza mama huyo wakati huo wakimkimbiza mtoto huyo kituo cha afya cha Kongowe kwa ajili ya matibabu ambapo anaendelea vizuri.
“Mtoto huyo alichukua mayai hayo akiwa anacheza na wenzake lakini yeye peke yake ndiye aliyeadhibiwa na wenzake hawakuchukuliwa hatua yoyote na ameshonwa nyuzi 12 utosini na nyuzi  nane karibu na sikio,” alisema Mavalla.
Aidha alisema kuwa mtuhumiwa huyo alibadilisha nguo akiwa na lengo la kutaka kukimbia na alipoulizwa kampiga mwanae na nini alisema kamchapa tu na fimbo.

Mwisho.