Na John Gagarini, Kibaha
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli amewataka
viongozi mbalimbali ambao wanashindwa kwenda na kasi ya awamu ya tano
wajitathmini kwa kujiondoa wenyewe endapo watashindwa kuwajibika.
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Bwawani wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Dk Magufuli alisema kuwa kiongozi ambaye ndani ya miezi kadhaa hadi mwaka hajui alichokifanya ni vema akajiondoa mwenyewe na asisubiri kuondolewa.
“Serikali ya awamu huu ni ya uwajibikaji na si kutaka kufaidi ukubwa kufanya kazi lengo kubwa likiwa ni kuwatumikia wananchi hasa wale wanyonge ambao wanahitaji huduma zetu kwa kuwatumikia,” alisema Dk Magufuli.
Alisema kuwa kwa sasa tumeweka utaratibu wa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na si matumboni bali ziguse maslahi ya wananchi wengi.
“Fedha hizo si matumboni, semina wala posho au safari za nje ambapo nimepata mialiko zaidi ya 50 ya nje ya nchi lakini nimekataa kwenda nataka kwanza tunyooshane wenyewe kwanza maana nikitoka watajisahau,” alisema Dk Magufuli.
Aidha alisema kuwa baadhi ya viongozi waliotumia vibaya rasilimali atapambana nao kwani Tanzania haiwezi kuwa nchi maskini kwani ni nchi ya pili duniani baada ya Barazili kwa nchi zenye rasilimali nyingi duniani.
“Tunakila aina ya madini, wanyama, maji, maziwa na mlima mrefu Afrika haiwezekani kuwa wasindikizaji wa matarajiri na sisi ni matajiri haiwezekani watu wale mlo mmoja, wanakosa dawa na huduma nyingine hii haiwezekani tutahakikisha wananchi wanaishi maisha yanayoendana na hali halisi ya mali zetu naombeni mniombee,” alisema Dk Magufuli.
Alisema ataendelea kutumbua ambapo kwa sasa wachache wanalalamika na kulia ni wale waliokuwa wakijinufaisha huku wengi wakiumia huku wengine wakijinufaisha.
Alisema kuwa baadhi ya viongozi walishiriki kuhujumu nchi kwa kuingia mikataba mibovu hasa kwenye upande wa umeme ambapo baadhi ya walidiriki kusaini mikataba mibovu.
“Kwa sasa tuna mipango ya umeme wa uhakika ambapo nilipokwenda Ethiopia nilikutana na waziri mkuu nilimuuliza anafanyaje kupata umeme wa uhakika na kuuza nje tuliongea mengi na sasa wataalamu wake watakaja kwa ajili ya kuweka mazingira ya upatikanaji wa umeme wa uhakika,” alisema Dk Magufuli.
Akizungumzia kuhusiana na mauaji yanayoendelea wilaya za Kibiti na Rufiji alisema kuwa serikali ya awamu hii si ya kuchezea kwani wanaohusika wataona moto kwani watashughulikiwa kikamilifu.
“Tutawanyoosha na tayari tumeanza kuwanyoosha wanafikiri watapita hawatapita kikubwa kinachotakiwa ni wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua watu hao kwani baadhi ni ndugu jamaa na marafiki na kuendelea kuwaficha ni kujicheleweshea maendeleo ambapo kwa sasa wilaya hizo hazina viwanda kutokana na mauaji hayo,” alaisema Dk Magufuli.
Alibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana kwenye uongozi wake ni pamoja na makusanyo kuongezeka kutoka bilioni 880 na kufikia kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi ambapo fedha hizo zimeweza kulipa elimu bure, pensheni ambazo hazikulipwa tangu mwaka 2010.
“Tumeweza kulipa madeni ambayo yalifikia kiasi cha shilingi trilioni 1.3 sasa yaliyobaki ni bilioni mbili ambapo tutaendelea kulipa madeni hayo kwa watu mbalimbali wanaodai halali na siyo madeni hewa,” alisema Dk Magufuli.
Alibainisha kuwa kutokana na makusanyo hayo serikali imeweza kufuta ada kwenye shule za msingi na sekondari ambapo kwa sasa zinatolewa kiasi cha shilingi bilioni 81.7 kwa ajili ya uendeshaji wa shule.
“Kutokana na elimu bure idadi ya wanafunzi wa darsa la kwanza wanaoandikishwa kwenye shule ya msingi wamefikia milioni mbili toka milioni moja na wanaojiunga na shule za sekondari wamefikia asilimia 27 huku mikopo ya elimu ya juu ikiongezeka toka watu 95,000 hadi 125,000 na bajeti kwa sasa ni bilioni 483,” alisema Dk Magufuli.
Aliupongeza mkoa wa Pwani kuwa na viwanda vingi ambapo na kuwa moja ya mikoa ambayo imetekeleza agizo la kuwa na viwanda ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kuvutia uwekezaji.
Awali akimkaribisha Rais Dk Magufuli mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kwa sasa mkoa una viwanda 371 huku zaidi ya 80 vikiwa ni vikubwa na vya kati na vidogo 260.
Ndikilo alisema hata hivyo pamoja na mafanikio hayo changamoto kubwa ni upungufu wa umeme ambapo mahitaji ni megawati 60 lakini zinazopatikana ni 40, maji yasiyo na uhakika, baadhi ya maeneo kutokuwa na nishati ya gesi na baadhi ya barabara kutokuwa na lami.
Mwisho.