Monday, June 26, 2023

SERIKALI YATAHADHARISHA WANANCHI IRINGA KUACHA KUTEMBEA USIKU KUEPUKA ATHARI ZA KUVAMIWA NA SIMBA

SERIKALI imewatahadharisha Wananchi Mkoani Iringa kuacha kutembea usiku ili kuepukana na madhara ya kuvamiwa na Simba walioingia katika makazi ya watu.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Grace Tendega aliyetaka kujua nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wananchi wa Iringa wanaishi kwa uhuru kutokana na changamoto ya Uvamizi wa Simba.

“Niendelee kutoa elimu kupitia Bunge hili kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa Simba wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku lakini pia wenye mifugo wawashe mioto kuzunguka maeneo ya mifugo ili kuepusha Simba wasisogee katika maeneo yao” Mhe. Masanja amesisitiza.

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Masanja amesema Serikali tayari imeshapeleka helikopta inayozunguka usiku na mchana kuhakikisha Simba hao wanapatikana na kurudishwa katika maeneo yao ili kuhakikisha  maisha ya Watanzania yanalindwa kwa gharama yoyote

Kuhusu mikakati ya Serikali ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu, Mhe. Masanja amesema Serikali inatekeleza Mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mwaka 2020 – 2024 ambapo Wizara inatoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu; inajenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; kuwafunga mikanda (GPS collars) tembo; na kuanzisha timu maalum (Rapid response Teams).

Pia, Serikali inaendelea kuwashirikisha wananchi kwa kutoa mafunzo kwa Askari wa Vijiji (VGS) ili kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo katika maeneo ya wananchi.

Aidha, amesema Serikali imeshaweka mipango ya kujenga fensi ya umeme katika baadhi ya maeneo ili kupunguza athari ya wanyama wakali na waharibifu.

Thursday, June 22, 2023

*MAJALIWA APOKEA TAARIFA YA KAMATI MAALUM ALIYOIUNDA KUFUATILIA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA*


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo Alhamisi, Juni 21, 2023, Jijini Dodoma amepokea taarifa ya Kamati Maalum aliyoiunda kwa ajili ya kupitia, kuchambua na kutoa mapendekezo ya kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini. 

Taarifa hiyo imekabidhiwa na Mwenyekiti wa kamati, Dkt. John Jingu ambaye pia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, Waziri Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI, Angela

Kairuki, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Ahmad Chande, Makatibu Wakuu, Makamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanakamati na wataalam kutoka sekta mbalimbali za masuala ya kodi, biashara na uwekezaji.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Kamati hiyo imefanya kazi kubwa na imeleta majibu ambayo yatatatua changamoto za wafanyabiashara nchini na ameahidi kuwa Serikali imepokeat aarifa hiyo na itayafanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo.

Kamati hiyo ambayo ilipewa siku 14, imefanya mapitio katika maeneo mbalimbali ya kikodi, bandari na maeneo ya wafanyabiashara kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Sunday, June 18, 2023

TAASISI MWALIMU NYERERE YAFANIKISHA UPATIKANAJI DAMU









TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani imefanikisha upatikanaji wa damu uniti 32 ambazo zitatumika kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Akizungumza mara baada ya zoezi la uchangiaji damu lililofanywa kwa pamoja na Taasisi hiyo ya Nyerere kwa kushirikiana na Taasisi ya Chawa wa Mama Kibaha Vijijini  mgeni rasmi Yahaya Mbungulume ambaye alimwakilisha Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo alisema uniti hizo zitasaidia sana wagonjwa.

Mbungulume alisema kuwa zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwani limesaidia upatikanaji wa damu ambayo itasaidia wagonjwa wakiwemo wajawazito, wagonjwa na watu wanaopata ajali.

Kwa upande wake katibu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani Omary Pumzi alisema kuwa waliamua kujitolea damu baada ya kupita kwenye Hospitali na kuona jinsi gani kuna uhitaji mkubwa wa damu.

Pumzi alisema kuwa Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza malengo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya kukabilana na adui wa maendeleo ambao ni maradhi ujinga na umaskini hivyo afya ni moja ya malengo kwama yalivyo kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Naye mwenyekiti wa Chawa wa Mama Kibaha Vijijini Rehema Chuma alisema kuwa malengo ya taasisi yao ni kumsaidia Rais katika kuhakikisha nchi inapata maendeleo.

Akiongoza zoezi la uchangiaji damu Katibu Msaidizi wa Taasisi ya Mwalimu Taifa Neema Mkwachu alisema wanamuunga mkono Mwasisi wa Taifa kwa vitendo kwa kushiriki moja kwa moja.

Akielezea mafanikio ya zoezi la uchangiaji damu mratibu wa huduma za maabara Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Nabwike Mwairinga alisema kuwa wamepata uniti 32 kwenye zoezi hilo ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kwenye benki ya damu ambapo wanahitaji uniti 40 kwa kila mwezi.






Friday, June 16, 2023

MJEMA AWATAKA WANACCM WATEMBEE KIFUA MBELE

 

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi, Ndugu Sophia Mjema, amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kutembea kifua mbele akisema chama hicho kimenyoka na hakiyumbishwi.

Mjema ametoa kauli hiyo 15.6.2023 katika viwanja vya Mnarani mjini Mpwapwa Mkoani Dodoma akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, ndugu Daniel Chongolo.

Katika mkutano huo wa hadhara, Mjema amesema Chama Cha Mapunduzi chini ya Mwenyekiti wake Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kinaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi kwa vitendo.

Amewataka wana-CCM kutoogopa kukisemea chama chao hasa kwa watu wanaotosha miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na chama hicho kupitia Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

"Niwaambieni wananchi wa Mpwapwa mna chama imara sana, chama chemu ni sikivu kinasikiliza changamoto zenu na kuzitafutia ufumbuzi kupitia kwa watendaji mbalimbali wa serikali, hivyo ungeni mkono juhudi za serikali na msiwasikikize wapotoshaji.

Aidha, Mjema amesema CCM imenyooka kama rula na haiyumbishwi.

*MHE. MWINJUMA AFUNGUA MASHINDANO YA UMISSETA TABORA*

 

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma leo Juni 15, 2023 mkoani Tabora amefungua mashindano ya michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSSETA) kitaifa katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana  Tabora.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo Mhe. Mwinjuma amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya michezo nchini kwa kuanza na shule 56 za sekondari, mbili katika kila Mkoa, ili kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali

‘’Ndugu viongozi na wanamichezo Serikali kwa upande wake kupitia ushirikiano wa Wizara zetu tatu (Ya kwangu  Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMI)  imefanya jitihada kubwa katika kuimarisha shughuli za michezo katika shule za Msingi na Sekondari”amesema Mhe. Mwinjuma.

Mashindano hayo yatafanyika kwa siku saba yakihusisha timu za michezo  mbalimbali kutoka Mikoa 32 ya Tanzania bara na Zanzibar.

DK JAFO NCHI KUKABILI MABADILIKO TABIANCHI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wananchi hawana budi kushiriki katika zoezi la upandaji wa miti.

Amesema hayo leo Juni 15, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge wa Viti Maalumu Mhe. Mariamu Kisangi na Mhe. Jacqueline Msongozi waliouliza mikakati ya Serikali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo amesema kuwa kwa mujibu wa wataalamu wa hali ya hewa kiwango cha mvua kimeshuka kutokana na changamoto hiyo na kusababisha ukame katika baadhi ya maeneo yakiwemo mikoa ya Arusha na Manyara.

Hivyo, Serikali imeelekeza kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka na kuitunza ikiwa ni hatua ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Awali Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema amewahamasisha wananchi kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira ambazo husababisha mabadiliko ya tabianchi.

Amewaasa wananchi kuacha kukata miti ovyo, kuepuka kilimo kisicho endelevu katika vyanzo vya maji, kuepuka ufugaji unaoharibu mazingira pamoja na uvuvi haramu.

Naibu Waziri Khamis amesema kuwa Serikali inachukua hatua kwa kuanzisha na kutekeleza miradi ya kuzuia madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika jamii.

Aidha, amesema kuwa Serikali imeandaa Sera, Mikakati na Mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inatoa elimu na namna bora ya kukabiliana na athari hizo kwa wadau wote muhimu wakiwemo wananchi katika maeneo yote nchini


Thursday, June 15, 2023

𝗦𝗜𝗠𝗕𝗔𝗖𝗛𝗔𝗪𝗘𝗡𝗘 𝗔𝗜𝗣𝗢𝗡𝗚𝗘𝗭𝗔 𝗲-𝗚𝗔 𝗨𝗦𝗜𝗠𝗔𝗠𝗜𝗭𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗘𝗛𝗔𝗠𝗔 𝗦𝗘𝗥𝗜𝗞𝗔𝗟𝗜𝗡𝗜

 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kukuza na kuimarisha Serikali Mtandao nchini.

Mhe. Simbachawene alitoa pongezi hizo jana, alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka  ya Serikali Mtandao zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu ya e-GA katika usimamizi wa matumizi ya TEHAMA kwenye taasisi za umma.

Alisema kuwa, kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma, kunatokana na usimamizi mzuri wa e-GA katika kuimarisha jitihada za serikali mtandao, hali ambayo imesaidia kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji kazi wa shughuli za serikali pamoja na utoaji huduma kwa wananchi.

“Bila Serikali Mtandao mambo mengi yangekuwa hayaendi sawa, e-GA mmetumia teknolojia kurahisisha na kufanikisha shughuli nyingi za Serikali kufanyika kwa wakati pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, nawapongeza sana”, alisema.

Pamoja na pongezi hizo, pia Waziri aliitaka e-GA kuimarisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) ili kutengeneza vijana wengi zaidi ambao watabuni mifumo inayotatua changamoto zilizopo. 

“Ni muhimu kuimarisha kituo cha utafiti na ubunifu ili kuandaa na kutengeza vijana mahiri katika masuala ya teknolojia kwa maslahi mapana ya taifa, na sisi upande wa Wizara tutahakikisha tunatoa msaada wa kutosha pale mtakapohitaji”, alisema.

Aidha, aliitaka e-GA kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuhakikisha wanapata mafunzo ya muda mfupi na mrefu kutoka ndani na nje ya nchi, ili kuwaongeza ujuzi wa kukabiliana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia katika usanifu wa mifumo, miundombinu pamoja na miradi ya TEHAMA yenye tija kwa taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu e-GA Eng. Benedict Ndomba, alimshukuru Waziri kwa kufanya ziara hiyo pamoja na ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka Wizarani katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

Alisema kuwa e-GA itaendelea kuimarisha kituo cha utafiti na ubunifu pamoja na kutoa elimu kwa Taasisi za Umma katika usimamizi na uzingatiaji wa Sheria, kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao ili kuhakikisha mifumo na miradi yote ya TEHAMA katika taasisi za umma inakuwa na tija kwa taifa.