Wednesday, October 1, 2025

WAWEKEZAJI WAITWA WAZAWA WAPEWA KIPAUMBELE HEKARI 100 ZATENGWA KONGANI YA KWALA.

WATANZANIA wametakiwa kwenda kuwekeza kwenye eneo la Kwala Wilayani Kibaha ambapo zimetengwa hekari 100 wawekezaji wanapewa hekari moja bure na sharti ni mtaji pekee.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo cha Kwala Industry Park (KIP) Kaimu Meneja wa Mawasiliano kwa Umma na Habari Adelina Rushekya kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TISEZA) amesema kuwa wanawahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa hiyo ya uwekezaji.

Rushekya amesema kuwa wameanzisha kampeni ya kuwataka Watanzania kuwekeza kwenye maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji ikiwemo Kongani ya Viwanda Kwala badala ya kuwaachia wageni kufanya uwekezaji.

"Hadi sasa kuna wawekezaji 10 wameonyesha nia ya kuwekeza wengi wakiwa ni wazawa pamoja na wageni ambapo wawekezaji hao wameonyesha nia kuwekeza kwenye sekta za kilimo, umeme jua na vifaa vya majumbani,"amesema Rushekya.

Naye msimamizi wa kiwanda cha kuunganisha majokofucha Snowsea Tanzania Co Ltd kilichopo kwenye eneo la kituo hicho cha Uwekezaji cha Kwala Gerald Tilia amesema kuwa wana uwezo wa kuunganisha majokofu 10 hadi 15 kwa siku.

Tilia amesema kuwa wafanyakazi wanaofanya kazi hiyo ya kuunganisha majokofu ni wazawa baada ya kupatiwa mafunzo kutoka kwa Wachina na hadi sasa kuna wafanyakazi 30.