Thursday, September 12, 2019

CCM YACHANGIA MABATI 500 ELIMISHA KIBAHA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)Taifa kimekabidhi mabati 500 kwa ajili ya kuunga mkono kampeni ya wilaya ya Kibaha ya Elimisha Kibaha yenye lengo la kujenga madarasa ili kukabiliana na changamoto upungufu wa madarasa 65 unayoikabili wilaya hiyo.

Akikamkabidhi mabati hayo mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama ambaye ndiyo muasisi wa kampeni hiyo katibu Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole alisema kuwa wameamua kuunga mkono kampeni hiyo ambayo inaisaidia serikali na inatekeleza ilani ya chama ambayo inatekelezwa na Rais ya kutoa elimu bila ya malipo kwa shule za msingi na sekondari.

Polepole alisema kuwa  tangu Rais Dk John Magufuli alivyotangaza elimu bure kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi zaidi ya mara tatu na hivyo kuongeza mahitaji ya uhaba wa madarasa, madawati na walimu ambalo serikali inalifanyia kazi na wamesha ongea na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) ili Kibaha ipewe kipaumbele kwenye mgawanyo wa walimu.

“Wakuu wa chama wamefurahi sana kwa hili lililofanywa na waliridhia mimi kuja kushiriki nanyi na tunapopata watendaji na viongozi wa serikali wanaojituma wanapaswa kuungwa mkono na kusimama nao na ndiyo tuliweka ahadi ya chama ya kuchangia mabati 600 na tumeanza na mabati 500 kwa awamu hii ya kwanza na awamu ya pili tutatoa mabati 100 na mifuko ya saruji 100,” alisema Polepole.

Alisema kuwa wanafurahishwa na kazi inayofanyika kwani inatekeleza ilani ya chama na uongozi wa wilaya umepanda mbegu bora kwani kwani mkuu wa wilaya ya Kibaha amepanda kitu kizuri na viongozi wengine wamepata hamasa kwani wameanza kufanya kama yeye hiyo ni hamasa si lazima kusubiri fedha ya serikali kwani wananchi wako tayari kuchangia maendeleo yao wenyewe.

“Tunataka viongozi wahamasishe umma kama ulivyofanya wewe angalia tumeokoa shilingi ngapi kwa jitihada mlizozifanya kwa madarasa 26 ya mwanzo kati ya 65 yanayotarajiwa kujengwa kupitia kampeni hiyo ambapo fedha zilizookolewa zitakwenda kusaidia wale ambao hawajaweza kufanya kama mlivyofanya nyie Kibaha huu ndiyo uongozi unaotakiwa,” alisema Polepole.

Alisema viongozi wanapaswa kufanya mambo mema ya maendeleo kama hakuna watu wanaowaona hiyo ndiyo tafsiri ya uongozi au mtumishi mwadilifu usifanye ili watu waone kwani watakuwa si waadilifu bali wafanye kama jambo binafsi fanya kama lako mwenyewe na wakipatikana viongozi kama hao ambapo wapo tayari watamsaidia Rais kwa ndoto za kuibadilisha nchi zitatimia mapema kabla ya muda.

Awali mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama alisema kuwa baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika hivi karibuni walipata vifaa na fedha zilizokusanywa vitatosha ujenzi wa madarasa 26 kwa Halmashauri mbili za Kibaha Mjini na Wilaya ya Kibaha ambapo kila moja imeanza ujenzi wa madarasa 13.

Mshama alisema kuwa ujenzi wa madarasa hayo umeanza baada ya wakurugenzi wa Halmashauri hizo kupatiwa vifaa vya ujenzi ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa 65 ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 1.3 na hii imetokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu darasa la saba.

Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaofaulu darasa la saba ambapo kwa mwaka 2017 jumla ya wanafunzi walifaulu 3,560, mwaka 2018 wanafunzi 3,938 walifaulu na mwaka 2019 wanafunzi waliongezeka na kufika 4,930 hali ambayo imesababisha kuwa na upungufu mkubwa wa madarasa hayo yanayohitajika.

Mwisho.