Na John Gagarini, Bagamoyo
WILAYA ya Bagamoyo mkoa Pwani imeweka mkakati wa kuhakikisha
wanafunzi wote waliopata nafasi ya kwenda sekondari wilayani humo wanakwenda
shule na kuondokana na dhana kuwa mkoa huo hauna mwamko wa elimu.
Hayo yalisemwa na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Bw Ahmed Kipozi wakati
wa mahafali ya 22 ya shule ya sekondari ya Lugoba na kusema kuwa tayari
wameshakutana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali na
wazazi ili kufanikisha suala hilo.
Kipozi alibainisha kuwa moja ya mkakati huo ni ule wa ujenzi
wa hosteli kwenye baadhi ya maeneo ili kuwapunguzia umbali wanafunzi ambapo
moja ya changamoto imeonyesha kuwa umbali nao umekuwa chanzo cha wanafunzi
kutopenda shule.
“Kwa sasa tumeunganisha nguvu ya pamoja na wadau wa elimu
ndani ya wilaya ili kuhakikisha malengo ya watoto kwenda shule kwa kiwango
kikubwa yanafikiwa ambapo washikadau wametuunga mkono na tunaamini mabadiliko
yanaonekana kama leo unavyoona watoto wengi wamemaliza elimu yao ya sekondari,”
alisema Bw Kipozi.
Awali mwalimu mkuu wa wa shule hiyo Bw Alhaj Abdalla Sakasa
alisema kuwa anaomba wadau wa elimu kujitokeza kuwasaidia kupata fedha kwa
ajili ya kugharamia vifaa vya maabara na kemikali kwa ajili ya wanafunzi wa
kidato cha nne na cha sita kwani gharama ni kubwa sana.
Alhaj Sakasa alisema kuwa shule yake ina wanafunzi wengi wa
masomo ya Sayansi hivyo kufanya maandalizi ya na kuendesha mitihani hiyo ya
kitaifa kutumia gharama kubwa ambazo kwa sasa hawana.
“Gharama kwa wanafunzi wa kidato cha nne ni shilingi milioni
5.8 na kidato cha sita ni shilingi milioni 7 ambazo hadi sasa hatuna licha ya
kuwa serikali inatoa ruzuku lakini ni kidogo sana ukilinganisha na gharama halisi,” alisema
Alhaj Sakasa.
Aidha alisema kuwa wazazi wengi hawana uwezo wa kulipia
chakula kama ilivyoamuriwa ambapo kila mwanafunzi anapaswa kuchangia kiasi cha
shilingi 100,000 kwa muhula ambazo wazazi wanshindwa kulipa.
Aliongeza kuwa wanampongeza mlezi wa shule hiyo Bw Subbash
Patel kwa kuisaidia shule na watumishi wa shule ambapo aliwasaidia vifaa vya
ujenzi na baadhi wamefanikiwa kujenga nyumba zao za kuishi, Katika mahafali
hayo jumla ya wanafunzi 212 walipewa vyeti vya kuhitimu kidato cha nne ambapo
shule hiyo ina wanafunzi 1,228 na walimu 57.
Mwisho.